Kikosi cha klabu ya Yanga sc kimewasili jijini Kigali Rwanda kwa ajili ya mchezo wa raundi ya pili ya michuano ya klabu binngwa barani Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan utakaofanyika siku ya Jumamosi saa kumi jioni kwa saa za Tanzania.
Mchezo huo utafanyika katika uwanja wa Nyamirambo jijini ambapo tayari umekua gumzo jijini humo kutokana na umati wa mashabiki kutoka jijini Dar es salaam wameambatana na timu hiyo kuhakikisha ushindi unapatikana.
Kikosi hicho kimetua mapema kikiwa na mastaa kamili kasoro nahodha Bakari Mwamnyeto ambaye ana matatizo ya kifamilia huku Stephane Aziz Ki na Djigui Diarra wakiwa tayari wamewasili mapema nchini humo wakitokea katika timu zao za Taifa moja kwa moja.
Rais wa timu hiyo Hersi Said, Meneja wa timu Walter Harson, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam, Lameck Nyambaya walikuwepo katika msafara huo ambapo Meneja wa timu walter Harrison alisema kuwa kila kitu kipo sawa kwa upande wao.
“Bakari Mwamnyeto tayari tumetoa taarifa yake tangu asubuhi kuwa hatokuwepo kutokana na matatizo ya kifamilia huku Aziz na Diarra wenyewe tayari wapo Kigali kabla yetu na watakua sehemu ya kikosi huku pia hali ya kikosi kizima iko salama na tumeajiandaa” Alisema meneja huyo.
“Tunamshukuru mungu tumesafiri salama kutoka Dar es salaam na kama Tff tupo tayari kuhakikisha timu inapata ushindi siku ya Jumamosi huku tunaowaomba mashabiki watuunge mkono kwa wingi siku ya mchezo”Alisema Lameck Nyambaya
Yanga sc inapambana ili kumaliza ukame wa kutofuzu hatua ya makundi ya kombe la klabu bingwa barani Afrika ambapo mara ya mwisho walifuzu mwaka 1998.