Kocha Roberto Oliveira wa Simba sc ameamua kumpa mkataba mpya beki wa klabu hiyo Erasto Nyoni ili awe kiongozi wa wachezaji wenzie kutokana na kupevuka kwake awapo uwanjani huku akibebwa na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja klabuni hapo.
Awali kulikua na mpango wa kumtema staa huyo kutokana na umri kumtupa mkono lakini kocha huyo raia wa Brazil ameona kuwa ni muhimu kuwa na wakongwe kikosini ili kuwaongoza vijana waliopo klabuni hapo.
Simba sc ipo kwenye maboresho makubwa ya kikosi cha timu hiyo ambapo baadhi ya mastaa wanatemwa huku tayari Augustine Okrah akiwa ameshaachwa na wengine kama Gadiel Michael,Joash Onyango,Victor Akpan wakifuatia huku kubaki kwa Nyoni kukiwa gumzo.
“Kocha anataka Nyoni awe kiongozi wa wachezaji wenzake, anamuona akili yake imekomaa na ana maamuzi anayoweza akawasaidia wengine kukaa kwenye njia sahihi, kutokana na umri wake, amesisitiza wasije wakamuachia aondoke,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kiluichongeza;
“Nyoni ni mchezaji anaweza akawakemea wadogo zake wanapofanya sivyo,hana mambo mengi ya kumfanya awe na nidhamu mbovu, jambo ambalo kocha anaona kuwepo kwake kikosini kutaongeza utulivu kwa wengine kuzingatia nidhamu na kujituma kwenye majukumu yao.”
“Ukiachana na nidhamu ya Nyoni ambayo ipo wazi, kocha anapenda uwezo wake anaoweza akacheza zaidi ya nafasi moja, anaona amejitunza kwa umri wake angekuwa hana nidhamu angekuwa ameishaondoka kwenye mstari.
Nyoni alijiunga na Simba sc mwaka 2017 akitokea klabu ya Azam Fc ambapo alijiunga kutokea timu ya Vital O ya Burundi na kudumu hapo kwa miaka saba.