Klabu ya Yanga sc inahitaji alama tatu pekee kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la shirikisho baada ya jana kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Real Bamako katika mchezo wa nne wa makundi michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.
Ikianza na mabadiliko machache ya Aziz Ki baadala ya Khalid Aucho ambaye alikua ametoka katika majeraha ambapo dakika za mwanzo ilifanikiwa kumiliki mchezo na kushambulia kwa kasi hatimaye kufanikiwa kupata bao la uongozi la Fiston Mayele dakika ya nane ambaye alipokea pasi ya upendo kutoka kwa Kennedy Musonda.
Baada ya bao hilo Real Bamako walizinduka na kumiliki mchezo huku Yanga sc wakipoteana eneo la katikati mwa uwanja na kukaribisha mashambulizi kadhaa ambayo hayakuzaa goli kutokana na safu ya ushambuliaji ya wageni kutokua imara.
Kipindi cha pili Yanga sc walifanya mabadiliko wakimuingiza Khalid Aucho kuchukua nafasi ya Stephane Aziz Ki huku Jesus Moloko akiingia badala ya Tuisila Kisinda ambapo dakika ya 68 Moloko aliipatia Yanga sc bao la pili na la mwisho katika mchezo huo.
Katika mchezo wa Kundi D wa mapema Tp Mazembe ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Us Monastry na kufanya msimamo wa kundi hilo kuongozwa na waarabu hao wakiwa na alama 10 huku Yanga sc wakiwa nafasi ya pili kwa alama 7 na Real Bamako akiwa na alama 2 na Mazembe wakiwa na alama tatu.
Yanga sc inapaswa kushinda mchezo dhidi ya Us Monastry utakaofanyika nchini Machi 19 ili kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.