Video inayosambaa mitandaoni ikimuonyesha mama mzazi wa kiungo wa Yanga sc Feisal Salum imezua taharuki miongoni mwa wadau wa soka nchini kutokana na madai ya mzazi huyo kuwa mchezaji huyo alipata mateso makubwa alipokua akiitumikia klabu ya Yanga sc kabla ya kuamua kuvunja mkataba wake hivi karibuni.
Mama mzazi huyo alisema kuwa mwanae alipitia wakati mgumu kiasi cha kula ugali na sukari wakati akiitumikia klabu hiyo hivyo wao kama familia hawana mpango wa kuendelea na klabu hiyo na wako nyuma ya mtoto wao katika jambo hilo.
“Fei kapata manyanyaso sana mpaka hapa ilipofikia imenibidi niyaweke wazi mambo ikiwa tayari tarehe ya kusikilizwa kwa shauri lake TFF imefika naomba shirikisho litoe haki maana katika kutetea haki yake Fei kafikia hatua ya kula ugali kwa sukari”
Hata hivyo tayari kamati ya sheria na hadhi za wachezaji imekaa mapema hivi leo na kusikiliza shauri hilo ambapo Feisal alifika akiambatana na wanasheria wake Nduruma Majembe na Fatma Karume pamoja na familia huku upande wa Yanga sc ukiwakilishwa na mkurugenzi wa sheria wa klabu hiyo Saimon Patrick na mtendaji mkuu wa klabu hiyo Andre Mtine.
“Tuliitwa kwenye review na tumekuja, tumesikilizwa na kusikiliza na sasa tunasubiri jibu la kamati tu,” alisema Mtine.
Mpaka sasa bado kamati hiyo haijatoa majibu ya mwisho ya shauri hilo baada ya kusikilizwa kwa pande zote mbili huku ikitarajiwa kuwa mapema taarifa rasmi itatoka kuhusu uamuzi wa kamati hiyo.