Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kuchukua alama tatu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Klabu ya Simba Sc katika mchezo uliofanyika Jumamosi Oktoba 19 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Simba sc chini ya Kocha Fadlu Davis ulianzisha kikosi chake kile kile kilichovuna alama 13 katika michezo mitano ya ligi kuu huku Lionel Ateba akiwa mshambuliaji namba moja akisaidiwa na Jean Charles Ahoua,Joshua Mutale na Kibu Dennis huku viungo wakiwa ni Yusuph Kagoma na Deborah Fernández na ukuta ukiongozwa na Che Malone Fondoh na Abdulrazak Hamza na pembeni wakicheza Shomari Kapombe na Mohammed Hussein na golini akianza Moussa Camara.
Kocha wa timu ya Yanga sc Miguel Gamondi yeye alianza n Djigui Diarra,Yao Kouasi Attouhoula,Chadrack Boka huku mabeki wa kati wakiwa ni Ibrahim Hamad Bacca na Dickson Job wakisaidiwa na viungo Khalid Aucho na Mudathir Yahaya huku pembeni wakiwacheza Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli na Prince Dube sambamba na Stephan Aziz Ki wakiongoza eneo la ushambuliaji.
Simba sc walianza na kasi kubwa kusukuma mashambulizi mengi langoni mwa Yanga sc lakini Uimara wa kipa Djigui Diarra uliwanyima bao la wazi dakika ya tano ya mchezo akiokoa mpira hatari wa Ateba.
Pia Kibu Dennis alikua mwiba kwa mabeki wa Yanga sc ambapo mwamuzi Ramadhan Kayoko alilazimika kusimama imara mara kadhaa kutokana na staa huyo kuchezewa faulo nyingi ambazo moja ilidhaniwa kuwa penati.
Yanga sc walijibu mashambulizi kwa Maxi Nzengeli na Aziz Ki kukosa nafasi za wazi mara moja huku Abdulrazak Hamza akishukuru kudra za mwamuzi Kayoko asipewe kadi nyekundu baada ya kumzuia Dube kwa faulo akiwa kama mtu wa mwisho.
Dakika za mwishoni mwa mchezo refa Kayoko aliamuru faulo ipigwe kuelekea lango la Simba sc baada ya Augustine Okejepha kumchezea madhambi Kennedy Musonda ambapo faulo hiyo iliyopigwa na Chama iliokolewa vibaya na kipa Camara na kumkuta Nzengeli aliyepiga langoni na Kelvin Kijiri kujifunga bao pekee la mchezo huo.
Dakika tisini zilimalizika vibaya kwa Simba sc kupoteza mchezo huo licha ya kucheza vizuri tofauti na mechi zilizopita za wababe hao wa kariakoo.
Yanga sc sasa imefikisha alama 15 ikicheza michezo mitano ya ligi kuu huku Simba sc ikisalia na alama 13 ikicheza michezo sita ya ligi kuu ya Nbc nchini.