Mwenyekiti wa klabu ya Simba Murtaza Mangungu amesema kuwa hali za kiafya za wachezaji na wafanyakazi waliokumbwa na mlipuko wa homa ya mafua ndani ya kikosi chao hali iliyopelekea mchezo wao dhidi ya Kagera sugar kuahirishwa.
Mangungu amesema kuwa wachezaji hao wanaendelea vizuri na matibabu pamoja na kuendelea na mazoezi yao kama kawaida kujiandaa na michezo iliyopo mbele yao kwenye michuano mbalimbali kama ligi kuu ya NBC na kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu ndani ya visiwa vya karafuu Zanzibar.
Kufuatia kuripoti idadi kubwa ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kupatwa na shida ya mafua na matatizo ya kupumua,bodi ya ligi iliamua kuuahirisha mchezo huo ili kudhibiti usambaaji zaidi wa mlipuko huo ulioshika kwa kiasi kikubwa nchini ndani ya wiki za hivi karibuni.
Simba kwasasa wanajiandaa na mchezo wa ligi kuu ya NBC dhidi ya KMC na watasafiri hadi Tabora ambako ndiko utakaofanyika katika dimba la Ali Hasan Mwinyi.KMC ndio watakuwa wenyeji wa mchezo huo wakitumia kanuni za ligi zinazoruhusu timu kucheza mechi mbili za nyumbani nje ya uwanja wao ambao umezoeleka,hii ni mara pili kwa KMC msimu huu baada ya awali kuupeleka mchezo wao wa ligi dhidi ya Yanga huko Songea katikadimba la Majimaji.
Katika hatua nyingine Mangungu amezungumzia maendeleo ya zoezi la uchangiaji wa fedha kwaajili ya ujenzi wa uwanja wa timu hiyo,amesema mpaka sasa unaendelea vizuri na wao kama viongozi wameshangazwa na muitikio mkubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa muitikio mkubwa.Pia watatengeneza kamati maalumu itakayoandaa michoro na bajeti ili kurahisisha.
Simba pia wataandaa mpango mzuri wa kuchangia kwa wale walio nje ya nchi,lakini pia wataanza kuwatambua wale watakaochangia kiasi kikubwa cha fedha.