Klabu ya soka ya Simba imepata ushindi mnono wa magoli 4-1 dhidi ya KMC katika mfululizo wa mechi za ligi kuu soka ya NBC inayoendelea hapa nchini na kujikusanyia pointi tatu muhimu katika harakati zake za kutetea taji la ligi kuu.
Mabingwa hao watetezi waliokwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 2-1 kwa magoli ya mapema kabisa kutoka kwa nahodha wa mchezo huo Mohamed Husein dakika ya 11 ,na lile la Joash Onyango kwa kichwa kunako dakika ya 13.Goli la KMC liliwekwa kimiani na Hassan dakika ya 40.
Kipindi cha pili Simba walianza tena kwa kiasi kutafuta bao la kuumaliza mchezo,na kunako dakika 46 ya mshambuliaji Kibu Denis aliipatia klabu yake goli la tatu kutokana na kutumia vema makosa ya walinzi wa KMC walioshindwa kuondoa mpira wa adhabu uliopigwa na Shomari Kapombe.Kibu aliiandikia timu yake goli linguine la nne dakika 57 ya kwa shuti kali nje ya 18.
Katika mchezo huo tukio lililowaacha midomo wazi wadau wengi wa soka ni lile la kocha mkuu wa timu hiyo Pablo Franco kumzuia Wawa kuingia uwanjani wakati tayari mwamuzi wa akiba alishanyanyua kibao kuonesha anapaswa kuingia,hata hivyo baadae ilikuja kujulikana kuwa mwamuzi kutoelewa maagizo toka benchi la ufundi la Simba.
Simba wamefikisha alama 21 katika msimamo wa ligi kuu baada ya michezo tisa,ponti mbili nyuma ya vinara Yanga wenye alama 23.Wekundu hao wa Msimbazi watarejea Dar es salaam kutoka Tabora ili kujiandaa na mchezo wao wa ligi dhidi ya Azam fc Januari Mosi kabla ya kuelekea Zanzibar kushiriki kombe la Mapinduzi.