Soka
MAURIZIO SARRI KUIBUKIA JUVENTUS
KOCHA Maurizio Sarri, ambaye ametwaa kombe la Europa League msimu huu akiwa na Chelsea, inasemekana ameshafikia muafaka na Juventus kwa ajili ya kuinoa timu hiyo kwa msimu ujao wa 2019/20.
Juventus inataka kumchukua Sarri kutoka Chelsea ili kuchukua nafasi ya Massimiliano Allegri, ambaye anaondoka mwishoni mwa msimu huu.
Sarri amebakiza miaka miwili katika mkataba wake wa kuinoa Chelsea, ambayo haijaweka wazi mustakabali wake.
Chelsea ilimchukua Sarri kutoka Napoli, ambayo ilikuwa inamlipa mshahara wa pauni milioni 5.4 kwa mwaka.
Juventus sasa ipo tayari kumwongezea kiasi cha pauni milioni 1.2 katika mshahara wake wa sasa, ambapo inasemekana Sarri amekubaliana nao.
Viongozi wa Juventus wana kazi ya kukubaliana na Chelsea ili kumalizana.
Hata hivyo, Juventus inatajwa pia kumfuatilia kocha wa Tottenham Hotspur, Mauricio Pochettino.
Hata hivyo, kuna ugumu wa kumpata Pochettino kwa kuwa klabu yake ya Tottenham Hotspur haitakuwa tayari kumwachia kirahisi kutokana na mafanikio aliyowapa..