Connect with us

Soka

Kocha Black Stars Aanza Kazi

Kocha mpya wa klabu ya Singida Black Stars Hamdi Miloud ameanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi hicho wiki hii baada ya kutambulishwa rasmi wiki iliyopita akichukua nafasi ya Patrick Aussems ambaye alitimuliwa klabuni hapo.

Miloud aliwasili nchini mapema ambapo baada ya kumalizana na mabosi wa klabu hiyo alipata nafasi ya kuishuhudia timu hiyo katika michezo kadhaa ya ligi kuu huku uongozi ukishughulikia vibali vyake vya kazi.

Baada ya Bodi  ya ligi kuu nchini kutangaza kusimama kwa ligi kuu kwa miezi miwili kocha huyo ameanza rasmi kuifundisha timu hiyo huku akijiandaa kuweka kambi maalumu jijini Arusha ili kuwanoa mastaa hao.

Kocha huyo alitambulishwa rasmi mbele ya wasaidizi wake aliowakuta akiwemo David Ouma sambamba na wachezaji wa kikosi hicho ambapo alisema anatarajia kupata ushirikiano mzuri ili kuleta ushindani kikosini humo.

“Ninafuraha kubwa kuwa hapa nanyi, pamoja nimekuja na msaidizi wangu Omar, Renaud, na timu nzima. Zimepita siku chache tangu nijiunge nanyi, na nimeweza kuona kuwa nyinyi ni watu wa maana sana ambao mnataka kuona na kupata matokeo bora kwa kila mmoja wenu.”Alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.

“Wakati wa kukaa kwangu hapa, nimekuwa na mikutano mingi nanyi, na hiyo imenipa imani zaidi katika uwezo wenu. Nina hakika kwamba kwa kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana kwa ufanisi, tunaweza kufanikisha mambo makubwa kwa pamoja. Nimekuwa na nafasi ya kufuatilia Michezo minne na kupata uzoefu ambao sasa nataka tushiriki kwa pamoja kuyaendea mafanikio ya klabu hii.”Alimalizia kusema

Kocha huyo ana uzoefu mkubwa wa kufundisha soka barani Afrika akiwa amewahi kufundisha vilabu vya Usm Algers,Nahdat Berkane,Cs Constantine na Js Kabylie.

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Soka