Timu ya soka ya KCCA kutoka nchini Uganda wamefanikiwa kuwa mabingwa wa michuano ya kombe la Kagame baada ya jana kuifunga timu ya Azm fc katika mchezo wa fainali uliochezwa katika uwanja wa Kigali nchini Rwanda.
Katika pambano hilo lililokuwa na kasi huku Azam fc wakionekana kupania kulipa kisasi cha kufungwa 1-o na KCCA katika hatua ya makundi,iliwachukua KCCA dakika 62 kupata bao lililofungwa na Mustapha Chiza na kudumu mpaka mwisho wa mchezo na kuwafanya Azam Fc kupoteza taji hilo walilolichukua mara mbili mfululizo.
MUSONYE AKOMAA NA SIMBA,YANGA.
Kitendo cha kutoshiriki michuano hiyo kwa timu za Simba na Yanga kimeonekana kutomfurahisha katibu mkuu wa Cecafa Nicholaus Musonye ambae amedai timu hizo kutoshiriki hakujaathiri kitu chochote na kuzitaka klabu hizo ziendelee kuzunguka nchi zingine na kuacha michuano katika ukanda wao.
“Nawaambia Simba na Yanga kwamba hata kama hawakuja watambue sisi hatukumuomba mtu, tuna timu nyingi sana za kujaza nafasi hizo. Wao waende huko Afrika Kusini, Uturuki wakaangalie majumba na takataka zingine zilizopo huko“, amesema Musonye.
“Kwanza kuna pre-season gani nzuri ambayo walitakiwa kuwa nayo zaidi ya hii?, yaani unaogopa kushindana, unakwenda kucheza mechi za kirafiki ambazo hazina maana. Serikali ya Rwanda imeandaa kila kitu hapa imesema njooni mcheze, wewe hutaki unakwenda Afrika Kusini kutembea”, ameongeza katibu mwenye maneno mengi.
Michuano ya Kagame hufanyika kila mwaka mwishoni mwa msimu na hudhaminiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwaka huu ilifanyika nchini humo na Kcca kuwa mabingwa huku Green Eagles ikishika nafasi ya tatu.