Akiwa bado hana hata wiki mbili tangu arejee klabu ya Yanga, kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima amesema wamedhamiria kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Niyonzima alijiunga na Yanga Alhamisi iliyopita na siku ya Jumamosi akacheza mechi dhidi ya Simba akiwa mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2
Niyonzima amesema amekuja nchini kuisaidia Yanga kurejesha ubingwa wa ligi kuu walioupoteza kwa watani zao Simba kwa misimu miwili sasa
Pamoja na kukiri kuwa wanahitaji kufanya kazi ya ziada kuwapoka ubingwa Simba, lakini wamejipanga
“Simba wana timu nzuri pengine kuliko hata nilipokuwa nikicheza msimu uliopita. Walitupa changamoto kubwa tulipocheza nao wiki iliyopita, Lakini juhudi za wachezaji pamoja na uzoefu vilituwezesha kusawazisha mabao mwili waliyotufunga,” amesema
“Tunafahamu tutapata upinzani mkali kutoka kwao na timu nyingine lakini tutapambana ili kuhakikisha tunafanikisha dhamira yetu”.
Niyonzima ni mmoja wa wachezaji wapya watano waliosajiliwa na Yanga dirisha dogo ili kukiongezea nguvu kikosi hicho.
Wengine ni Ditram Nchimbi, Tariq Seif, Yikpe Gnamien na Adeyum Saleh.
Yanga pia imemleta mshambuliaji Owe Bonyanga kutoka klabu ya TP Mazembe ambaye pia huenda akasajiliwa kuchukua nafasi ya David Molinga.