CHELSEA na Arsenal zinavaana leo Jumatano kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Europa itakayopigwa kwenye Uwanja wa Olimpiki mjini Baku katika nchi ya Azerbajain.
Mchezo huu ni muhimu zaidi kwa Arsenal kwani ikitwaa taji hili itapata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu kutoka Jiji la London kukutana katika fainali ya mashindano ya klabu barani Ulaya.
Hata hivyo, ni mara ya tatu kwa timu kutoka England kukutana katika fainali ya mashindano ya Ulaya wakati mara ya mwisho ikiwa miaka 11 iliyopita.
Chelsea haijapoteza mechi katika mashindano ya msimu huu ya Ligi ya Europa ikiwa imeshinda mechi 11 na kutoka sare tatu.
Wakati Arsenal ilipoteza mechi mbili za mashindano hayo msimu huu baada ya kufungwa na BATE Borisov na Rennes.
Timu hizi mbili zimewahi kukutana siku za nyuma katika michuano ya Ulaya wakati Chelsea ilipoitoa Arsenal kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2003/04.
Chelsea ilifungwa kwa penalti na Manchester United katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008.
Pia Chelsea ilitolewa na Manchester United kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2010/11.
Arsenal kwa upande wao wana rekodi mbovu wanapokutana na timu za England kwenye michuano ya Ulaya, ambapo iliwahi kutolewa na Liverpool na Manchester United kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa nyakati tofauti.
Hata hivyo, Arsenal ina rekodi nzuri likija suala la kushiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwani wameshiriki mara 19 mfululizo hadi msimu uliopita walipokosa na kushiriki Ligi ya Europa.
Msimu uliopita, Arsenal iliishia nusu fainali ya Ligi ya Europa, ambapo walitolewa na Atletico Madrid waliotwaa taji hilo msimu huo wa 2017/18.
Timu hiyo iliwahi kufika fainali ya Kombe la UEFA katika msimu wa 1999/2000, ambapo ilifungwa kwa penalti na Galatasaray.
Rekodi ya siku za nyuma kwa Chelsea ya kucheza katika fainali ya mashindano ya klabu barani Ulaya inaonyesha imeshinda mechi tano na imepoteza tatu.
Arsenal ina rekodi ya kutwaa taji la mashindano ya klabu barani Ulaya mara moja.
Timu hiyo imewahi kuingia katika fainali mara sita lakini mara moja tu ndio imeibuka kidedea.
Kocha wa Arsenal, Unai Emery amesema amepanga kuwaanzisha mastaa wake, Mesut Ozil na Pierre-Emerick Aubameyang kwenye mchezo huo.
Anaamini mastaa hao watasaidia katika mchezo huo, ambao ni muhimu sana kwa timu hiyo.
Staa wa Chelsea, Eden Hazard naye anatazamiwa kuiongoza timu yake kwa mara ya mwisho, ambapo atapania kuwapa taji kwani msimu ujao anatazamiwa kujiunga na Real Madrid.