Viongozi wa Simba wapo kwenye mipango kabambe ya kuhakikisha wanasajili straika mwingine wa kimataifa mwenye uwezo wa kufunga mabao zaidi ya Mnyarwanda, Meddie Kagere.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo ikose Kombe la Mapinduzi ambalo lilikwenda Mtibwa Sugar baada ya kuwafunga Simba bao 1-0 ambalo lilifungwa na Awadh Juma.
Timu hiyo hadi hivi sasa tayari imefanikiwa kumsajili kiungo mshambuliaji raia wa Msumbiji, Luiz Miquissione aliyekuwa anakipiga UD Songo kwa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns ya Afrika.
Uwezo wa Kagere umeshuka kwa kiasi kikubwa kwa sasa na hivyo uongozi unaona ni kutokana na kutumika sana katika mechi ambazo amezicheza hivyo anahitaji kupumzika.
Ukiachana na Kagere, Bocco naye ambaye ni kati ya washambuliaji tegemeo bado hajawa fiti kwa asilimia kubwa licha ya kupona hivyo ni ngumu kumtegemea ni lazima wasajili mshambuliaji mwingine wa kimataifa atakayekuja kuchukua nafasi ya Wilker Da Silva, aliyesitishiwa mkataba hivi karibuni.
Hivyo upo uwezekano mkubwa kabla ya dirisha la usajili halijafungwa Simba wakafunga usajili na mshambuliaji mmoja wa kimataifa kutoka nje ya nchi lakini pia inaelezwa kuwa wametishwa na kiwango cha Yanga cha sasa .
Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa timu hiyo Senzo Mazingisa hivi karibuni alisema kuwa timu hiyo ipo kwenye mipango ya kusajili wachezaji katika dirisha dogo kama kocha akitoa mapendekezo.