KLABU za Ligi Kuu Kenya (KPL) zimetakiwa zijitayarishe kwa nyakati ngumu zaidi kwa sababu hakuna matumaini ya mdhamini mpya kupatikana hadi ligi hiyo ikamilike msimu huu. Mwenyekiti wa KPL Ambrose Rachier alisema kwamba hakuna matumaini ya kupata mdhamini mpya na wale walioonyesha nia, walikuwa wakitoa pesa kidogo ambazo hazikutosha kuendesha ligi na kufadhili timu zote 18.
Kwa mujibu wa Rachier ambaye pia ni mwenyekiti wa Gor Mahia, walishindwa kuafikiana na kampuni hizo zilizotoa hela kiasi kidogo, kwa sababu zilidai mechi za KPL hazirushwi katika vyombo vya habari vya kimataifa. Hata hivyo, hakufafanua iwapo KPL inafaa kusimamishwa kwa sababu taji la msimu huu bado halijanunuliwa na pia itakuwa vigumu kumpa mshindi zawadi yake kwa sababu ya ukosefu wa mdhamini. Pia ikumbukwe kuwa washindi wa taji la msimu uliopita Gor Mahia bado hawajapewa zawadi zao hadi leo.
“Ligi ya KPL iko mashakani na hali ya sasa huenda isibadilike. Hakuna dalili zozote kwamba ligi itapata mdhamini msimu huu. Waliotaka kuidhamini walikuwa wakitoa pesa kidogo ambazo hazitoshi klabu zote 18. Vilevile walilalamik kwamba hawangepata faida sana kwa sababu mechi zetu hazirushwi kwenye runinga mbalimbali za kimataifa kama za nchi nyingine. Ni hali ya kusikitisha lakini hatuna budi ila kuikubali,” akasema Rachier.
Alithibitisha kwamba KPL ililazimika kuhamisha ofisi zake kutoka Westlands hadi barabara ya Lenana ili kupunguza gharama ya matumizi kwa sababu haingeweza kumudu kodi inayotozwa. Kauli ya Rachier inajiri baada ya timu tatu za KPL kukosa kufika uwanjani katika mechi sita huku Nzoia Sugar FC ikiwa timu ya hivi punde kukosa mechi yao dhidi ya Bandari, mjini Mombasa wikendi iliyopita. .
SoNy Sugar ambayo ilikosa mechi zake tatu dhidi ya Zoo Kericho, Tusker na AFC Leopards tayari imeondolewa kwenye ligi hiyo huku Chemeli iliyopata ushindi wake wa kwanza msimu huu kwa kuichapa Nzoia 1-0 ikikosa mechi dhidi ya Bandari na KCB.
Nb:Habari kwa msaada wa Dominick Salamba