Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msola ametoa ufafanuzi juu ya mapato ya matumizi tangu walipoingia madarakani mwezi Juni mwaka huu huku akisema hakuna pesa inayoliwa.
Msola amesema gharama za kuendesha timu ni kubwa kuliko mapato yanayoingia huku wakiwa wamerithi madeni makubwa kutoka katika uongozi uliopita.
Mwenyekiti huyo ametaja madeni makubwa ya aina nne waliyoyarithi ambayo ni kama ifuatavyo:-
1. Serikali (Mamlaka ya Mapato Tanzania ‘TRA’ shilingi milioni 800), 2.Ada ya uhamisho ya wachezaji shilingi waliosajiliwa miaka miwili ilyopita shilingi milioni 254.
3. Madeni ya makocha na wachezaji waliopita (Hans Van Pluijm, George Lwandamina, Youthe Rostand, Donald Ngoma na Obrey Chirwa) jumla shilingi milioni 600.
4. Watu binafsi shilingi milioni 237
5. Gharama za Usajili wa timu za wakubwa na ile ya Wanawake shilingi milioni 600.
Msola ametaja vyanzo vya mapato vya klabu hiyo ambayo ni SportPesa, KCB, Vodacom, Azam TV, GSM, Yanga TV na kampuni ya Maji ya Afya ambayo kwa mwaka wanapata shilingi bilioni mbili wakati gharama za kuiendesha timu ni bilioni nne. “Nimeamua kuja kwenu Waandishi ili nitoe ufafanuzi juu ya mapato na matumizi ya klabu yetu. Tulivyoingia madarakani tulikuta timu madeni makubwa ambayo tumejitahidi kuyapunguza huku bado tukitakiwa kuiendesha timu,” alisema Msola.