Kikosi cha Yanga sc jana kimepanda ndege kwenda nchini Zambia kucheza mchezo wa marudiano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya klabu bingwa barani Afrika dhidi ya Zesco United ya Zambia katika mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Levy Mwanawasa jumamosi hii.
Kikosi hicho chenye wachezaji 23 na Viongozi saba kimesafiri kwa mafungu ambao kundi la kwanza liliondoka jana saa mbili asubuhi na huku wengine wakiondoka jana saa mbili usiku.
Katika msafara huo wachezaji Issa Bigirimana na Paulo Godfrey waliachwa kutokana na majeraha huku Mustapha Selemani na David Molinga wakiachwa kutokana na kutopata leseni ya kucheza michuano hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa klabu hiyo Dk Mshindo Msola kikosi hicho kimeondoka na vyakula pamoja na maji ili kupekua hujuma.
“Tunatazama uwezekano wa kubeba chakula chetu pamoja na maji kwa lengo la kuepuka usumbufu wa mahitaji hayo pindi tutakapokuwa Zambia, kama tunavyofahamu mechi zetu za Afrika huwa na figisu figisu nyingi, hivyo hatutaki kuyumba na ndiyo maana tunataka kwenda Zambia tukiwa kamili,” alisema Msolla
Yanga ina kazi kubwa ya kupindua matokea ugenini baada ya kuruhusu sare ya 1-1 hapa nyumbani na kwa mujibu wa rekodi Zesco haijawahi kupoteza mchezo katika uwanja wa nyumbani na ili yanga isonge mbele inahitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 na kuendelea.