Timu za soka za Tanzania na Kenya zimeanza vibaya mechi za ufunguzi za kombe la mataifa ya Afrika baada ya zote kukubali kipigo cha mabao mawili kwa bila dhidi ya Senegal na Algeria na kuzifanya timu hizo zishike nafasi mbili za mwisho katika msimamo wa kundi C.
Tanzania iliwavaa senegal waliokuwa bila mshambuliaji wao hatari Sadio Mane ambaye alikua na kadi mbili za njano hivyo kutoruhusiwa kucheza mchezo huo ilianza mchezo kwa kujilinda zaidi ili kuwazuia Senegal waliokua wanalisakama lango la Taifa stars baada ya kuwazidi eneo la kiungo huku Feisal Salum na Mudathir Yahaya wasijue la kufanya kuwadhibiti viungo wa Senegal wakiongozwa Idrissa Gueye aliyekua hatari na kusababisha pasi ya goli la kwanza lililofungwa na Keita Balde Diao winga wa intermilan ya Italia.
Staa wa stars Mbwana Samata alishindwa kufurukuta mbele ya beki wa Napoli ya Italia Kalidou Coulibary aliyekua imara kumdhibiti huku Msuva na John Bocco wakiachwa yatima hali iliyowafanya watumia muda mwingi kurudi nyuma kusaidia viungo.
Keprin Diatta mwenye miaka 20 anayeichezea Club Brugge ya Ubelgiji aliachia mkwaju hatari dakika ya 68 na kuwapa senegali goli la pili lililodumu mpaka mwisho wa mchezo.
Harambee stars nao hawakuwa mbali na majirani zao wa Tanzania baada ya kukubali kipigo cha mabao mawili kwa bila kutoka kwa Algeria mabao ya Baghdad Bounedjah dakika ya 34 kwa mkwaju wa penati na Riyad Mahrez aliyefunga dakika ya 43.
Harambee stars waliofuzu michuano hiyo baada ya miaka 15 kupita walishindwa kufurukuta mbela ya Algeria waliokuwa wanashambulia muda wote wa mchezo na kumfanya mshambuliaji Michael Olunga kuwa mtalii katika goli la Algeria.
Mechi za kundi hilo zitaendelea tena Alhamisi ambapo Tanzania na Kenya zitakutana huku Algeria akikutana na Senegal.Atakayepoteza mchezo kati ya Tanzania na Kenya atakua amejihakikishia kurudi nyumbani mapema huku mshindi kati ya Algeria na Senegal atakua amefuzu kwenda hatua inayofuatia.