Mfanyabiashara nguli na maarufu nchini Tanzania Rostam Aziz amesema yupo tayari kuidhamini na kuendelea kuisaidia Yanga kwa maana ndio klabu anayoishabikia toka utotoni japo hayupo tayari kuwa mfadhili au mwekezaji pekee katika klabu hiyo.
Tajiri huyo ambaye ni kada wa chama cha mapinduzi(ccm) alisema kuwa Yanga ni timu ya wananchi hivyo inapaswa kuendeshwa na wananchi wenyewe kuliko kumpa mtu mmoja aindeshe timu hiyo kama mali yake binafsi kwani kufanya hivyo ni kuwanyima fursa wanachama na wananchi wengine kuisaidia timu yao.
”Njia sahihi ni wanachama wote wawe na mamlaka kuiendesha timu yao kupitia michango, wadhamini kupitia makampuni,TV rights na gate collection na kuuza bidhaa mbalimbali zenye nembo yetu”.
Pia bilionea huyo namba mbili nchini kwa mujibu wa jarida la forbes alisisitiza kuwa yupo tayari kuichangia timu hiyo kwa kuwapeleka viongozi nje ya nchi ili wakapate ujuzi ama kuleta wataalamu nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao.
Bilionea huyo ambaye alikua mbunge kwa miaka kadhaa aliamua kukutana na waandishi wa habari baada ya hivi karibuni taarifa kusambaa kuwa ana mpango wa kuwekeza ndani ya klabu hiyo japo leo hii amekanusha taarifa hizo na kusisitiza yupo tayari kuwa mdhamini wa kawaida tu kupitia moja ya makampuni yake.