Goli la dakika ya 71 la Clement Mzize limefanikiwa kuiokoa Yanga sc na kupata alama tatu katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union uliofanyika katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Yanga sc ikianza na mastaa wale wale walioiua Simba sc kwa mabao 5-1 isipokua Djigui Diarra na Joyce Lomalisa pamoja na Nahodha Bakari Mwamnyeto ilifanikiwa kuimilika Coastal ambao muda mwingi walikaa nyuma ya mpira.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga sc ilionekana kukosa maarifa ya kuivuka safu ya ulinzi ya Coastal iliyokua chini ya Lameck Lawi ambapo Kennedy Musonda na Aziz Ki walikosa maarifa ya kuivuka safu hiyo ya ulinzi.
Kipindi cha pili Kocha Miguel Gamondi aliwatambulisha mchezoni Jesus Moloko na Clement Mzize ambaye alifanikiwa kufunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Moloko aliyepokea pasi ya Stephane Aziz Ki.
Yanga sc sasa ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ya Nbc wakiwa na alama 24 huku Coastal Union wakisalia katika nafasi ya 13 wakiwa na alama saba katika michezo tisa ya ligi kuu nchini.