Klabu ya Azam Fc imeshindwa kuchukua alama tatu muhimu katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini dhidi ya Klabu ya Namungo Fc uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex Chamazi baada ya kubanwa na kutoa sare ya 1-1.
Azam Fc ilishindwa kufurukuta baada ya kuruhusu bao la mapema la Hamis Halifa Nyenye dakika ya 12 kwa shuti kali lililomshinda kipa Mohamed Mustapha.
Bao halikudumu sana kwa jitihada binafsi za Feisal Salum zilisaidia kumpa pasi nzuri Gibril Sillah na kufunga bao zuri dakika ya 44 ya kipindi cha kwanza.
Baada ya kutoka mapumziko mechi iliendelea kuwa nzuri na ya kuvutia huku Azam Fc wakikosa penati baada ya kipa Jonathan Nahimana kuokoa penati ya Feisal Salum.
Mpaka dakika 90 zinakamilika timu hizo ziligawana alama na Azam Fc kufikisha alama 45 katika michezo 22 nafasi ya 3 ya msimamo huku Namungo Fc wakifikisha alama 23 katika michezo 22 ya ligi kuu katika nafasi ya 12 ya msimamo.