Klabu ya Yanga sc imefanikiwa kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Nbc baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Namungo Fc katika mchezo wa ligi kuu nchini uliofanyika katika uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Yanga sc iliyoanza na kikosi kile kile kilichocheza na Al Merrekh isipokua Mudathir Yahaya ambaye alianzia benchi huku Kennedy Musonda akianza pamoja na mshambuliaji Clement Mzize huku Pacome na Aziz K wakiwa kama viungo sambamba na Max Nzengeli na Khalid Aucho.
Kocha Cedrick Kaze aliamua kuanza na viungo wengi eneo la katikati ili kuwadhibiti Yanga sc ambapo Jacob Massawe,Erasto Nyoni,Frank Domayo,Hashim Manyanya na Pius Buswita walikua eneo hilo na kufanikiwa kuziba nafasi kwa viungo wa Yanga sc ambao walibanwa karibuni katika kila eneo la uwanja.
Pamoja na kazi nzuri ya viungo wa Namungo Fc kuwadhibiti Yanga sc bado pia ubutu wa safu ya ushambuliaji ya Yanga sc ilionekana wazi kwani Mzize,Max na Musonda kwa nyakati tofauti walikosa magoli ya wazi.
Kipindi cha pili kocha wa Yanga sc alimuingiza Mudathir kuchukua nafasi ya Pacome Zouzou ambapo kuingia kwa kiungo huyo kuliongeza kasi ya ushambuliaji na hatimaye dakika ya 87 ya mchezo pasi ya Aziz Ki ilimkuta beki Yao Yao ambaye alimpasi Mudathir Yahaya aliyefunga bao la ushindi.
Mwalimu Miguel Gamondi anastahili pongezi kutokana na kiwango cha mastaa wake huku mabadiliko yake ya kuwaingiza Mudathir na Jesus Moloko yalizaa matunda kwa wote kushiriki katika upatikanaji wa bao hilo.
Yanga sc sasa ipo kileleni mwa msimamo wa ligi kuu nchini ikiwa na alama tisa na mabao kumi na moja ya kufunga ikiwa haijafungwa bao lolote mpaka sasa.