Kocha Juma Mgunda amekubali kubeba lawama katika mchezo dhidi ya Azam Fc ambao ulimalizika kwa klabu ya Simba sc kukubali kipigo cha 1-0 kutoka kwa Azam Fc ikiwa ni ushindi kwa Azam Fc baada ya miaka sita tangu wapate ushindi dhidi ya wekundu hao wa msimbazi.
Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na Prince Dube dakika ya 35 ya mchezo akipokea pasi ya upendo kutoka kwa James Akaminko pembeni ya uwanja ambapo alimchungulia kipa Aishi Manula alipokaa na kupiga mpira kuelekea pembeni ya goli na kuzua shangwe mwa mashabiki wa Azam Fc ambao waliungana na mashabiki wa Yanga sc kushangilia ushindi huo.
Azam Fc ilianza na Dube kama mshambuliaji pekee huku ikijaza viungo wengi eneo la katikati mwa uwanja na kuwazidi ujanja Simba sc ambao walianza na safu ya Mkude na Kapama kama viungo wa chini huku juu wakicheza Chama na Okra na Moses Phiri na Habib Kyombo akicheza kama mshambuliaji pekee dhidi ya mabeki Edward Manyama na Daniel Amoah.
Kufuatia kipigo hicho kocha Juma Mgunda akiongea na waandishi wa habari baada ya mchezo huo alikubali matokeo huku akisema kuwa lawama wasitupiwe wachezaji wake bali atupiwe yeye kama kocha wa klabu ambapo unakuwa ni mchezo wa kwanza kwa Simba kupoteza msimu wa 2022/23 na ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa Kocha Mkuu, Juma Mgunda kuonja joto ya jiwe ya kupoteza pointi tatu.