Klabu za Simba Sc na Kmc zimeingia katika mgogoro kuhusu usajili wa kiungo mshambuliaji Awesu Awesu ambaye tayari ametambulishwa na Simba Sc akijiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.
Kmc wamesisitiza kuwa usajili huo ni batili kwa kuwa mchezaji huyo ana mkataba na klabu hiyo wa miaka mwaka mmoja utakaoisha mwaka 2015 huku wakipinga utaratibu uliotumika wa mchezaji huyo kurejesha kiasi cha shilingi milioni 50 ili kununua mkataba wake kama kipengele cha kuvunja mkataba kinavyosema.
“Huu ni uhuni ambao hauna nafasi kwenye mpira wetu kwasasa, hili sio suala la ubabe bali suala la kisheria, sisi tunapeleka suala kwenye mamlaka husika wao watakuja na mkataba wao na sisi tutakuja na mkataba wetu, tumeshangaa sana Simba kumtangaza Mchezaji wetu pasipo na kuzungumza na sisi kufanya biashara yoyote”Alisema mtendaji mkuu wa klabu ya Kmc Daniel Mwakasungula.
Kwa upande wa Simba sc wanasisitiza kuwa wao walichofanya ni kumsajili mchezaji huyo akiwa huru baada ya kuvunja mkataba wake na Kmc kwa kutekeleza yale yaliyomo katika mkataba huo hivyo hawahusiki na mgogoro huo.
Hoja kubwa ya Kmc ni kuwa mchezaji alipaswa kuijulisha klabu kama kuna ofa ndipo klabu hizo zikubaliane kuvunja mkataba huo ndipo mchezaji huyo asaini huko kuliko hivi sasa ambapo wanahoji Simba sc imepata wapi ruhusa ya kuzungumza na mchezaji moja kwa moja bila kupitia kwa klabu.
Kmc tayari imeamua kuripoti suala hilo katika mamlaka ya soka nchini (TFF) ambapo sasa watasubiri kikao cha kamati ya sheria na hadhi za wachezaji kuja kutoa muongozo ama uamuzi wa nani mwenye haki.