Wachezaji wanne wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wataukosa mchezo wa Alhamisi dhidi ya Benin kuwania tiketi ya kufuzu michuano ya kombe la dunia Qatar 2022 kutokana na sababu mbali.
Wachezaji hao ni mabeki Erasto Nyoni,Bakari Mwamnyeto,Shomari Kapombe na kiungo Jonas Mkude.
Mwamyeto na Kapombe wataukosa mchezo huo kutokana na majeraha waliyopata hivi karibuni wakivitumikia vilabu vyao huku Erasto Nyoni sababu ikiwa haiko wazi japo inasemekana naye ni matatizo ya kiafya.
Maswali mengi ya wadau wa soka nchini yamekuwa ni kwa kiungo Jonas Mkude ambaye taarifa kutoka kwa Meneja wa Taifa Stars Nadir Haroub mchezaji huyo aliomba ruhusa na kuruhusiwa kutokana na sababu za kifamilia,lakini cha kushangaza ni kuonekana kwake kwenye mazoezi ya klabu yake ya Simba huko Bunju.
Tetesi zinadai kuwa mchezaji huyo ameondolewa Stars kutokana na sababu za kinidhamu japo hazijaanishwa ni zipi.