Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanikiwa kufuzu kushiriki michuano ya mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2025 baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Guinea kwa bao 1-0 katika mchezo mgumu wa kuwania kufuzu kupitia kundi H.
Stars ilikua lazima ishinde ili kupata nafasi ya kufuzu ambapo Guinea walikua na alama 9 huku Stars wakiwa na alama 7 na mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ulikua wa mwisho katika kundi hilo huku Dr Congo akiwa tayari ameshafuzu kwa alama 12 kileleni mwa msimamo wa kundi hilo.
Kwa kujua umuhimu wa ushindi katika mchezo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk Samia Suluhu Hassan alitoa ofa ya mashabiki kuingia bure ili kuongeza hamasa kwa wachezaji.
Kocha wa Stars Hemed Moroco alifanya mabadiliko machache kutoka katika kikosi kulichoshinda 2-0 dhidi ya Ethiopia ambapo alimuanzisha staa wa Azam Fc Adolph Mtasingwa akichukua nafasi ya Novatus Dismas huku mabeki wakiwa ni Shomari Kapombe,Mohammed Hussein,Dickson Job na Ibrahim Hamad Bacca ambapo kiungo alikua ni Mtasingwa na Mudathir Yahaya sambamba na Feisal Salum huku washambuliaji wakiwa ni Mbwana Samata,Simon Msuva na Clement Mzize.
Iliwalazimu Stars kumaliza kipindi cha kwanza matokeo yakiwa 0-0 ambapo mapema dakika ya 62 Simon Msuva alifunga bao pekee kwa mchezo huo ambalo lilidumu kwa dakika zote tisini.
Baada ya filimbi ya mwisho shangwe zilitawala uwanjani hapo ambapo sasa hii imekua mara ya nne kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo ikianza mwaka 1981,2019,2023 na hii ijayo itakayofanyika mwaka 2025 nchini Morocco.