Connect with us

Makala

SportsPesa Yakabidhi Mamilioni Yanga Sc

Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya Sportspesa imekabidhi hundi ya kiasi cha shilingi za Kitanzania 537,500,000 ikiwa ni sehemu ya Bonasi za klabu hiyo kutokana na kufanya vizuri katika msimu huu wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.

Kampuni hiyo ambayo ilisaini mkataba wa udhamini na klabu hiyo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 12.33 kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2022 ambapo pia kuna vipengele vya kuipatia bonasi klabu hiyo pindi inapofanya vizuri katika michuano ambayo inashiriki.

Yanga sc msimu huu imefanikiwa kuwa mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo wa ligi kuu nchini pamoja na kombe la shirikisho la Crdb huku pia ikifika hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la klabu bingwa barani Afrika ambapo ilitolewa na Mamelod Sundowns kwa matuta.

Makabidhiano ya mfano wa hundi hiyo yalifanyika katika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani ambapo Rais wa Yanga sc Eng.Hersi Said alihudhuria sambamba na Afisa Mtendaji mkuu Andre Mtine sambamba na uongozi wa kampuni ya Sportspesa.

“Leo tunakabidhi mfano wa Hundi kwa Klabu ya Young Africans SC kama BONUS ya mafanikio ya msimu. Hundi hii ina Thamani ya Tsh 537,500,000/= ambayo itawekwa kwenye akaunti za benki za Young Africans SC”Alisema mkurugenzi wa Oparesheni wa kampuni hiyo Mh.Abbas Tarimba

“Nawashukuru pia Wachezaji na benchi wa Young Africans SC kwa kile walichokifanya pale Zanzibar. Licha ya Wachezaji wetu wawili muhimu kukosa penati za mwanzo bado hawakupoteza malengo ya kuipambania nembo ya Klabu yetu” Alimalizia kusema mkurugenzi huyo ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha Jimbo la Kinondoni.

Naye Rais wa klabu ya Yanga sc aliwashukuru Sportspesa kwa kutekeleza yote ambayo walikubaliana katika mkataba huo wa miaka mitatu wakiwa kama wadhamini wakuu.

“Nikupongeza Mzee wangu Mhe. Abbas Tarimba kwa jitihada zako kwetu. Kila mara tulipokukimbilia hukuchelewa kutusikiliza. Nimpongeze sana na Mkurugenzi Pavel Slavkov kwa kutekeleza matakwa yote ya kimkataba ambayo yanaifanya Klabu hii kuwa imara zaidi pamoja na watendaji wote wa Sportpesa”Alisema Rais Hersi.

“Vile vile leo tumepokea bonus kutoka kwa Sportpesa, baada ya Young Africans SC kufika hatua ya Robo Fainali ya ligi ya Mabingwa barani Afrika. Sportpesa wametekeleza hitaji hili ambalo lipo kwenye mkataba wetu ambapo Sportspesa watapaswa kutoa bonus kwa Young Africans kwenye kila hatua watakayofika kwenye mashindano ya Kimataifa”Alimalizia kusema Hersi.

Yanga sc msimu huu umekua msimu wa mafanikio kama ilivyokua misimu miwili iliyopita ambapo imefanikiwa kuchukua makombe takribani yote nchini kwa misimu miwili iliyopita huku msimu huu ikichukua taji la ligi kuu ya Nbc na michuano ya kombe la Shirikisho sambamba na kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika.

 

Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

More in Makala