Kamati ya maadili ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) imewatoza faini ya shilingi milioni tano,ofisa habari wa Simba Sc, Haji Manara, ofisa habari wa Yanga Sc, Hassan Bumbuli pamoja na jumbe wa kamati ya sheria ya Shirikisho hilo, Zakaria Hanspope kutokana na makosa mbalimbali ya kimaadili.
Mwenyekiti wa kamati ya maadili TFF, Wakili Kichere Mwita Waissaka amesoma leo Septemba 14 uamuzi wa kamati hiyo makao makuu ya TFF mbele ya waandishi wa habari na kuweka wazi rufaa ,huku akiongeza kuwataka watatu hao kutofanya kosa lolote la kimaadili ndani ya miaka miwili.
Manara ambaye ni msemaji mkuu wa klabu ya Simba amekutwa na hatia ya kuingilia majukumu ya kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji wakati wa kesi ya mchezaji Bernard Morrison kwa maneno aliyoyatoa kupitia Wasafi Media.
Kwa upande wa Bumbuli amekutwa na hatia ya kusema uongo kwa kamati ya katiba, hheria na Hadhi za wachezaji kwamba hawajapeleka nakala ya hukumu ya kamati wakati nakala ilifikishwa kwenye klabu yake siku moja kabla ya yeye kuongea na Wasafi Media.
Hanspope ana hatia katika makosa mawili ambalo moja ni kutoa taarifa ya muenendo wa shauri ambalo lilikuwa linajadiliwa huku yeye akiwa ni mjumbe wa kamati hiyo na pili kuchochea umma kuhusu sakata la mchezaji Bernard Morrison.