Wachezaji wa klabu ya Simba sc wamepata zawadi ya kiasi cha shilingi za Kitanzania milioni tano ikiwa ni zawadi maalumu inayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa timu ambazo zinashiriki michuano ya kimataifa endapo zitapata goli katika michezo yake inayoendelea msiu huu.
Simba sc wanaoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika huku Yanga sc wakishiriki michuano ya kombe la shirikisho walipewa ahadi hiyo ya kununua kila goli kwa shilingi milioni tano kutoka kwa Rais ahadi ambayo tayari ameshaanza kuitekeleza ambapo Yanga sc walizawadiwa kiasi cha Shilingi milioni kumi na tano baada ya kushinda mabao 3-1 dhidi ya Tp Mazembe.
Msemaji mkuu wa serikali Mh.Gerson Msigwa amekabidhi fedha hizi kwa uongozi wa klabu ya Simba sc mapema baada ya kurejea nchini kwa niaba ya Mh.Rais Samia na ilipokelewa na nahodha wa klabu hiyo John Bocco mbele ya viongozi wa klabu hiyo Salim Abdalah “Try again” na Mangungu ambaye ni mwenyekiti wa klabu hiyo.
“Kwa niaba ya Mh.Rais ninakabidhi fedha hizi ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake kwa Simba sc na Yanga sc endapo watapata goli katika michuano ya kimataifa na hivyo nina furaha kukabidhi zawadi hii ya shilingi milioni tano”Alisema Msigwa ambaye ni msemaji mkuu wa serikali.
“Tunamshukuru sana Rais kwa zawadi hii inayoonyesha ni jinsi gani anathamini michezo na sisi kama wachezaji tunamuahidi hatutomuangusha tutaendelea kupambana”Alisema John Bocco nahodha wa klabu hiyo.
Simba sc wamepata zawadi hiyo baada ya kuifunga Vipers Fc 1-0 ugenini nchini Uganda ambapo walifanikiwa kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kupoteza dhidi ya Horoya Fc na Raja Casablanca mchezo uliofanyika nyumbani uwanja wa Benjamin Mkapa.