Simba Sc jana ilikuwa ikicheza na Namungo Fc uwanja wa taifa katika mechi ya michuano ya ligi kuu inayoendelea ambapo Simba wameibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo Fc.
Bao la kwanza Simba lilipatikana dakika ya 21 kupitia Francis Kahata ambalo lilisawazishwa na Bigirimana Blaise dakika ya 35 kutokea Namungo Fc huku Simba kabla ya kwenda mapumziko waliongeza bao la pili dakika ya 38 kupitia Hassan Dilunga.
Namungo walijipatia bao la pili dakika ya 70 kupitia Lusajo ambaye aliachia shuti kali akiwa nje ya 18 na kumfanya Kakolanya kuambulia kuokota mpira nyavuni.
Meddie Kagere ambaye ni mshambuliaji wa Simba aliwachapa Namungo bao la tatu dakika ya 88 na kuwafanya walale chali kwani alimaliza shughuli uwanjani kwa kufunga bao la ushindi ambalo limewapa timu yake pointi 3.
Simba inafikisha jumla ya pointi 44 ikiwa nafasi ya kwanza na imefunga jumla ya mabao 38.