Timu ya Taifa ya Cameroon imetolewa katika michuano ya Afcon 2021 baada ya kufungwa kwa mabao 3-1 kwa penati baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za mchezo huo wa nusu fainali uliofanyika katika Uwanja wa Paul Biya Jijini Yaoundé..
Licha ya kuwa na mastaa kama Vicent Abubakar,Toko Ekambi na Andre Onana bado Cameroon ilishindwa kupata bao dhidi ya Misri yenye Mohamed Salah na Mohamed Elneny katika eneo la kiungo kiasi cha kusababisha mchezo kusubiri kuamuliwa kwa matuta.
Kipa wa klabu ya Zamalek, Mohamed Abou Gaba ‘Gabaski’ ndiye aliyeibuka shujaa wa Mafarao kwa kucheza penalti mbili za nyota wa Simba Wasiofungika, Harold Moukoudi na James Lea Siliki, wakati mkwaju wa mchezaji wa zamani wa Tottenham Hotspur, Clinton N’Jie uliota mbaya.
Kocha wa Mreno wa Misri, Carlos Queiroz alitolewa kwa kadi nyekundu na refa Mgambia, Bakary Papa Gassama baada ya kupingana na maamuzi kipindi cha pili.
Sasa Misri itakutana na Senegal katika mchezo wa fainali siku ya Jumapili huku ikiwakutanisha mastaa wa Liverpool Sadio Mane na Mohamed Salah.