Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf) limeamuru mchezo wa fainali ya pili ya kombe la Shirikisho barani Afrika baina ya klabu ya Simba Sc dhidi ya Rs Berkane kuchezwa katika uwanja wa Amaani Complex Visiwani Zanzibar badala ya Benjamin Mkapa kama ilivyotarajiwa.
Mchezo huo uliopangwa kuchezwa hapa nchini Mei 25 2025 awali ilitarajiwa utafanyika jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Benjamin Mkapa lakini baada ya wakaguzi kutoka Caf kuukagua uwanja huo mara kwa mara wamejiridhisha kwamba haufai.
Sababu kubwa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wakaguzi hao ni kwamba sehemu ya kuchezea ya uwanja huo inahifadhi maji kipindi hichi cha mvua na hivyo mpira hautachezwa kwa utulivu mkubwa.
Mpaka sasa klabu ya Simba Sc na Serikali kupitia Shirikisho la Soka nchini (TFF) wameshapewa taarifa hiyo na wanajaribu kupambana kuona kama wanaweza kuwashawishi Caf kubadili uamuzi huo.
Endapo Caf itaendelea kushikilia msimamo huo maana yake ni kwamba Berkane watakua wamepata nafuu kutokana na uwanja wa Amaani Complex kuchukua idadi ndogo ya mashabiki tofauti na Benjamin Mkapa.