Ni ubabe kwa kwenda mbele ndio ulitawala katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini baina ya Tabora United dhidi ya Singida Black Stars uliofanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na kumalizika kwa sare ya 2-2.
Ubabe ulianza nje ya uwanja kwa wasemaji wa klabu hizo Hussein Masanza wa Singida Black Stars na Christina Mwagala wa Tabora United ambapo waliahidiana kuoana endapo Tabora ingefungwa huku Masanza akiahidi kuvaa wigi la Christina endapo Black Stars ingefungwa.
Ndani ya uwanja timu hizo zinazonolewa na makocha wa kigeni Patrick Aussems wa Singida Black Stars na Anicet Kiazayidi raia wa Congo Drc anayeinoa Tabora United.
Singida Black Stars ilikua ya kwanza kupata bao likifungwa na Elvis Rupia dakika ya 16 kwa kichwa akiunganisha krosi iliyoshindwa kuokolewa na mabeki wa Tabora United huku Anthony Bi Tra Bi akifunga bao la pili hivyo likitokana na uzembe wa mabeki wa Tabora United kuokoa mpira uliozagaa ndani ya eneo la 18 la timu hiyo.
Baada ya Mapumziko Tabora United walijipanga vizuri na kusawazisha mabao hayo kupitia kwa Yacouba Sogne dakika ya 46 na Heritier Makambo dakika ya 49 ya mchezo huo.
Baada ya matokeo kuwa sare ya 2-2,Timu hizo zilishambuliana kwa zamu lakini mpaka dakika 90 zinakamilika hakuna timu iliyoona lango la mwingine.
Kutokana na matokeo hayo Singida Black Stars imefikisha alama 24 katika nafasi ya nne ya msimamo huku Tabora United ikifikisha alama 18 katika nafasi ya tano ikicheza michezo 12 ya ligi kuu.