Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Yanga sc Pacome Zouzoua amezua kizaazaa baada ya kusua sua kusaini mkataba mpya klabuni hapo baada ya ule wa awali kuelekea ukingoni ambapo kuanzia Januari mwakani atakua huru kuanza mazungumzo na klabu nyingine.
Mabosi wa klabu hiyo tayari wameshaweka ofa yao mezani kwa mchezaji huyo lakini mpaka sasa anasuasua kukubaliana na ofa hiyo akisisitiza kutimiziwa baadhi ya mahitaji yake ikiwemo kiasi cha dau la usajili na mshahara.
Staa huyo anahitaji zaidi ya shilingi milioni 35 za kitanzania kama mshahara huku pia dau kubwa la usajili kitu ambacho kinawaumiza kichwa mabosi wa klabu hiyo.
Sambamba na hilo staa huyo inaelezwa yuko tayari kuanza mazungumzo na klabu za Simba na Azam Fc sambamba na baadhi ya klabu kutoka nje ya nchi ambazo zimeonyesha nia ya kumsajili zikiwasilisha ofa za maana.
Hali ipo tofauti kwa mchezaji mwingine wa klabu hiyo Yao Kouasi Attouhoula ambaye naye yupo kwenye mwaka wa mwisho wa mkataba wake ambapo yeye yuko tayari kusaini huku makubaliano kwa asilimia kubwa yakiwa yameshafikiwa.
Yao na Pacome Zouzoua walisajiliwa pamoja msimu wa 2021/2022 na baada ya kuonyesha viwango bora wote wawili wanahitajika kusalia klabuni hapo.