Baada ya kutoonekana katika kambi ya klabu ya Simba Sc ikidaiwa yuko mkoani Kigoma,Hatimaye staa wa klabu ya Simba Sc Kibu Dennis ameonekana akikwea Pipa kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kufanya majaribio katika timu kadhaa.
Kwa mujibu wa Viza aliyokata staa huyo inaonyesha kwamba ataenda nchini Norway kwa ajili ya majaribio kisha atakwenda pia nchini Sweden ambapo kuna timu inahitaji kumuangalia uwezo wake kabla ya kumsajili moja kwa moja.
Hata hivyo pamoja na kufanikiwa kuondoka nchini,Staa huyo atakutana na wakati mgumu pindi atakaporejea kutokana na kuondoka bila ruhusu ya waajiri wake klabu ya Simba Sc ambayo tayari imetoa taarifa kwa umma kuhusu kutoroka kwa mchezaji huyo ikisisitiza kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
“Klabu ya Simba inautaarifu umma kuwa mchezaji wetu Kibu Denis Prosper hajaripoti kambini kwaajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mwaka 2024-2025,” imeeleza na kuongeza,
“Tunapenda kuutarifu umma kuwa Simba tulimuongezea mkataba Kibu, mkataba wa miaka miwili zaidi utakaoisha Juni 2026 na kumlipa stahiki zake zote za kimkataba,”
“Hata hivyo mchezaji huyu amekuwa akitoa sababu kadhaa wa kadha zinazomfanya kushindwa kuripoti kambini, kutokana na utovu huu wa nidhamu klabu itamchukulia hatua stahiki za kinidhamu na umma utapewa taarifa.”Ilimalizia taarifa hiyo kupitia mtandao wa kijamii wa instagram.
Hata hivyo kwa upande wa wasimamizi wa mchezaji huyo kampuni ya Football Fraternity ikiwakilishwa na mtu aliyejitambulisha kama Rashid Yazid alisema kuwa mchezaji huyo amefanya kitendo cha utovu wa nidhamu huku akihisi kuwa mchezaji huyo ameshawishiwa kuchukua uamuzi huo.
“Mimi ndiye ninayetambulika na Simba Sc, nimeanza kumsimamia kuanzia dili lake la kwanza Simba Sc, awali nilikuwa mwanasheria ya Kibu tu kabla ya Jamal (aliyekuwa wakala wake) kunikabidhi baada ya kuwa na majukumu mengine nje ya Nchi.” Alisema Yazid
“Mchezaji ameshawishiwa na ametoroshwa kwenda Ulaya, mchezaji hana ‘technical know how’ yeye ni mtaalamu wa mpira! ameshawishiwa na kufanya mipango ya kuondoka kwenda Ulaya.”Alisitiza msimamizi huyo ambaye kitaaluma ni Mwanasheria
“Kilichotokea ni utovu wa nidhamu kwanza yeye kwenda Kigoma kwenda kumuuguza mzazi wake hakutoa taarifa kabla baadaye mimi niliitaarifu klabu juu ya suala la matatizo yake ya kifamilia…. Taarifa za kuuguliwa na mzazi alizitoa kwa kiongozi Simba ambaye sio sahihi.”Alimalizia kusema
Kibu Dennis alijiunga na Simba Sc misimu miwili iliyopita akitokea Mbeya City Fc ambapo msimu huu alisaini mkataba mpya wa miaka miwili klabuni hapo ambapo hajarejea mpaka sasa.