Timu ya Al Ahli Tripoli ya nchini Libya tayari imewasili salama jijini Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Simba SC mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Benjamin William Mkapa.
Klabu hiyo imekuja kwa tahadhari kubwa kutokana na kuhofia usalama wao hapa nchini ambapo baada ya kuwasili wamepokelewa na kampuni binafsi ya mabaunsa ilikulinda usalama wao nje ya uwanja hadi kufikia siku ya mchezo husika ambao utafanyika Jumapili ya Septemba 22.
Katika mchezo wa awali uliofanyika nchini Libya ambao uliisha kwa sare ya bila kufungana kulitokea vurugu ambapo mashabiki wa klabu hiyo licha ya kujitokeza kwa wingi pia waliwafanyia vurugu wachezaji wa klabu ya Simba Sc pamoja na mwamuzi.
Katika vurugu hizo mastaa walioathirika ni pamoja na Aishi Manula ambaye alipigwa akiwa jukwaani huku ikilazimu vyombo vya ulinzi kuingilia kati kuwanusuru mastaa wa Simba sc baada ya mchezo kumalizika ili warejee vyumbani na kisha hotelini.
Katika mchezo huu wa marudiano,Simba Sc inahitaji ushindi wa aina yeyote ili kufuzu ambapo ikifungwa ama kupata sare ya mabao basi itakua imetolewa katika michuano hiyo ya kombe la Shirikisho barani Afrika na kuhitimisha ndoto ya klabu hiyo ya kufika walau nusu fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu wa 2024/2025.