Baada ya klabu ya Yanga sc kumshtaki staa wake Feisal Salum kufuatilia staa huyo kuamua kuvunja mkataba na klabu hiyo na kulipa kiasi cha Tsh 112m ikiwa na dau la usajili na mishahara ya miezi mitatu na kisha kutimka klabuni hapo hatimaye suala hilo litaamuliwa siku ya Januari 6 katika ofisi za makao makuu ya shirikisho la soka nchini (Tff).
Tayari Shirikisho hilo kupitia kamati ya sheria na hadhi za wachezaji limemuandikia barua staa huyo kufika katika makao makuu hayo sambamba na wanasheria wake mapema siku hiyo ili kujibu shtaka hilo lililowasilishwa na klabu yake hiyo ikidai kuwa staa huyo amekiuka vifungu kadhaa katika mkataba huo.
Feisal alijiunga na Yanga sc msimu wa 2017/2018 na kisha alisaini mkataba mpya wa kuendelea kukipiga jagwani wa miaka minne mpaka june 30,2024 ambapo staa huyo kwa siku za karibuni alikua akidai kuongezewa mshahara lakini baada ya uongozi kutotimiza aliamua kuvunja mkataba huo.
Kwa sasa staa huyo yuko Dubai katika kambi ya mafunzo akijiweka fiti kujiandaa na majukumu mapya kama alivyobainisha yeye mwenyewe wakati akisafiri kuelekea nchini humo na tayari anatarajiwa kuwasili nchini kesho mapema tayari kuhudhuria shauri hilo ili kujua mbivu na mbichi.