Ndio msemo uliozagaa kwa mashabiki wa Yanga sc wakiwatambia mashabiki wa Simba sc baada ya kuibuka na alama tatau muhimu katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc uliofanyika katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam.
Ikiwakosa Khalid Aucho,Feisal Salum,Yannick Bangala na Farid Musa ambao kwa muda mrefu wamekua wakitawala eneo la kiungo la Yanga sc huku kwa mchezo huo ikiwaanzisha Zawadi Mauya na Abubakari Salum ilitosha kuwapa alama tatu ngumu licha ya timu hiyo kukutana na ugumu katika kufikisha mpira eneo la mwisho kwa Fiston Mayele na Saido Ntibanzokiza.
Iliwachukua Azam Fc dakika 10 kupata bao la kwanza kutokana na udhaifu wa eneo kiungo la Yanga sc ambalo lilikabia macho na kuruhusu pasi ya mpenyezo iliyomkuta Bruce Kangwa aliyepiga pasi kwa Rodgers Kola aliyefunga kwa shuti kali akimuacha kipa Djigui Diarra akiwa hana la kufanya.
Yanga sc walirudi mchezoni na kufanikiwa kusawazisha kwa penati kufuatia kipa Ahmed Salula wa Azam Fc kumuangusha Saido Ntibanzokiza na mpira wa penati uliopigwa na Djuma Shabani kujaa wavuni moja kwa moja na mpaka mpira unakwenda mapumziko kwa matokeo yakiwa 1-1.
Kipindi cha pili Yanga sc ilirudi kwa kasi na mipango mikali ya kusaka bao ambapo walifanikiwa kupata bao dakika ya 77 likifungwa na Fiston Mayele kwa shuti kali la kiki ya baiskeli na mpira kumshinda kipa Ahmed Salula kwa mara nyingine tena na kuwahakikishia mashabiki wa Yanga sc waliojaa chamazi kuondoka na alama tatu.
Fiston Mayele sasa anafikisha jumla ya mabao 11 kwenye ligi akiwa ni namba moja kwa watupiaji kwa msimu wa 2021/22 na anafuatiwa na Relliats Lusajo mwenye mabao 10 akiwa anakipiga Namungo FC yenye makazi yake mkoani Mtwara.
Yanga sc sasa imefikisha alama 51 ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu nchini ikifuatiwa na Simba sc ikiwa na alama 37 huku ikiwa na viporo vya michezo miwili ambapo timu hizo zitakutana mwishoni mwa msimu huu mechi ambayo itaamua kuwa Yanga sc ni mabingwa ama la kwa msimu huu.